1 BWANA ametamalaki, mataifa wanatetemeka;
Ameketi juu ya makerubi, nchi inatikisika.
2 BWANA ni mkuu katika Sayuni,
Naye ametukuka juu ya mataifa yote.
3 Na walisifu jina lake kuu litishalo;
Ndiye mtakatifu.
4 Mfalme mkuu upendaye hukumu kwa haki;
Umeiimarisha haki;
Umefanya hukumu na haki katika Israeli.
5 Mtukuzeni BWANA, Mungu wetu;
Sujuduni penye kiti cha miguu yake;
Ndiye mtakatifu.
6 Musa na Haruni walikuwa makuhani wake,
Na Samweli pia ni miongoni mwa walioliitia jina lake,
Walimlilia BWANA naye akawaitikia;
7 Akasema nao katika nguzo ya wingu.
Wakashika shuhuda zake na amri aliyowapa.
8 Ee BWANA, Mungu wetu, ndiwe uliyewajibu;
Ulikuwa kwao Mungu mwenye kusamehe
Ingawa uliwapatiliza matendo yao.
9 Mtukuzeni BWANA, Mungu wetu;
Sujuduni mkiukabili mlima wake mtakatifu;
Maana BWANA, Mungu wetu, ni mtakatifu.