1 Ee BWANA, usinilaumu katika ghadhabu yako,
Wala usiniadhibu kwa ukali wa hasira yako.
2 Kwa maana mishale yako imenichoma,
Na mkono wako umenipata.
3 Hamna uzima katika mwili wangu
Kwa sababu ya ghadhabu yako.
Wala hamna amani mifupani mwangu
Kwa sababu ya hatia zangu.
4 Maana dhambi zangu zimenifunika kichwa,
Kama mzigo mzito zimenilemea mno.
5 Majeraha yangu yananuka na kutunga usaha,
Kwa sababu ya upumbavu wangu.
6 Nimejipinda na kuinama sana,
Mchana kutwa ninaenda nikiomboleza.
7 Maana viuno vyangu vimejaa homa,
Wala hamna uzima katika mwili wangu.
8 Nimedhoofika na kupondeka sana,
Nimeugua kwa fadhaa ya moyo wangu.
9 Bwana, haja zangu zote ziko mbele zako,
Kuugua kwangu hakukusitirika kwako.
10 Moyo wangu unadundadunda,
Nguvu zangu zimenitoka;
Nuru ya macho yangu nayo imeniondoka.
11 Wanipendao na rafiki zangu wanasimama mbali na pigo langu;
Na jamaa zangu wanasimama mbali.
12 Nao wanaoutafuta uhai wangu hutega mitego;
Nao wanaotaka kunidhuru hunena mabaya;
Na kufikiri hila mchana kutwa.
13 Lakini kama kiziwi sisikii,
Nami ni kama bubu asiyefumbua kinywa chake.
14 Naam, nimekuwa kama mtu asiyesikia,
Ambaye hamna ubishi kinywani mwake.
15 Kwa kuwa nakungoja Wewe, BWANA,
Wewe utajibu, Ee Bwana, Mungu wangu.
16 Maana nilisema, Wasije wakanifurahia;
Wale wanaojitukuza juu yangu Mguu wangu unapoteleza.
17 Kwa maana mimi ni karibu na kusita,
Na maumivu yangu yako mbele yangu daima.
18 Kwa maana nitaungama uovu wangu,
Na kusikitika kwa dhambi zangu.
19 Lakini walio adui zangu bila sababu wana nguvu,
Nao wanaonichukia bure wamekuwa wengi.
20 Naam, wakilipa mabaya kwa mema,
Huwa adui zangu kwa kuwa nilifuata lililo jema.
21 Wewe, BWANA, usiniache,
Mungu wangu, usijitenge nami.
22 Ufanye haraka kunisaidia,
Ee Bwana, wokovu wangu.