1 Haleluya.
Heri mtu yule amchaye BWANA,
Apendezwaye sana na maagizo yake.
2 Wazawa wake watakuwa hodari duniani;
Kizazi cha wenye adili kitabarikiwa.
3 Nyumbani mwake mna utajiri na mali,
Na haki yake yadumu milele.
4 Nuru huwaangaza wenye adili gizani;
Ana fadhili na huruma na haki.
5 Heri atendaye fadhili na kukopesha;
Atengenezaye mambo yake kwa haki.
6 Kwa maana hataondoshwa kamwe;
Mwenye haki atakumbukwa milele.
7 Hataogopa habari mbaya;
Moyo wake u imara ukimtumainia BWANA.
8 Moyo wake umethibitika hataogopa,
Hata awaone watesi wake wameshindwa.
9 Ametoa kwa ukarimu, na kuwapa maskini,
Haki yake yakaa milele,
Pembe yake itatukuzwa kwa utukufu.
10 Asiye haki ataona na kusikitika,
Atasaga meno yake na kuondoka,
Matumaini ya wasio haki hupotea.