1 Heri aliyesamehewa dhambi,
Na kuondolewa makosa yake.
2 Heri ambaye BWANA hamhesabii hatia,
Na ambaye rohoni mwake hamna hila.
3 Nilipokosa kuungama dhambi zangu, mifupa yangu ilipooza
Kwa kulia kwangu mchana kutwa.
4 Kwa maana mchana na usiku
Mkono wako ulinilemea.
Jasho langu likakauka hata nikawa
Kama nchi kavu wakati wa kaskazi.
5 Ndipo nikakuungamia dhambi yangu,
Wala sikuuficha upotovu wangu.
Nilisema, Nitayakiri maasi yangu kwa BWANA,
Nawe ukanisamehe upotovu wa dhambi yangu.
6 Kwa hiyo, hebu kila akuaminiye
Akuombe awapo katika dhiki.
Hakika maji makuu yafurikapo,
Hayatamfikia yeye.
7 Kimbilio langu utanilinda nisipate mateso,
Utanizungusha nyimbo za kufurahia wokovu wangu.
8 Nitakufundisha na kukuonesha njia utakayoiendea;
Nitakushauri, jicho langu likikutazama.
9 Msiwe kama farasi wala nyumbu,
Wasiokuwa na akili.
Kwa matandiko ya lijamu na hatamu
Sharti kuwazuia hao, au hawatakukaribia.
10 Naye mtu mwovu ana mapigo mengi,
Bali amtumainiaye BWANA fadhili zitamzunguka.
11 Mfurahieni BWANA;
Shangilieni, enyi wenye haki
Pigeni vigelegele vya furaha;
Ninyi nyote mlio wanyofu wa moyo.