Publicidade

Salmos 74

Ombi la kutaka msaada wakati wa kushindwa
Utenzi wa Asafu.

1 Ee Mungu, mbona umetutupa milele?

Kwa nini hasira yako inatoka moshi

Juu ya kondoo wa malisho yako?

2 Ulikumbuke kusanyiko lako,

Ulilolinunua zamani.

Ulilolikomboa liwe kabila la urithi wako,

Mlima Sayuni ulioufanya maskani yako.

3 Upite na kupaona palipoharibika milele;

Adui ameufanya kila ubaya katika patakatifu.

4 Watesi wako wamenguruma kati ya kusanyiko lako;

Wameweka bendera zao ziwe alama.

5 Wanaonekana kama watu wainuao mashoka,

Waikate miti ya msituni.

6 Na sasa nakishi yake yote pia

Wanaivunjavunja kwa mashoka na nyundo.

7 Wamepatia moto patakatifu pako;

Wamelinajisi kao la jina lako hata chini.

8 Walisema mioyoni mwao,

Na tuwaangamize kabisa;

Mahali penye mikutano ya Mungu

Wamepachoma moto katika nchi pia.

9 Hatuzioni ishara zetu, wala sasa hakuna nabii,

Wala kwetu hakuna ajuaye, hadi lini?

10 Ee Mungu, mtesi atalaumu hata lini?

Adui alidharau jina lako hata milele?

11 Mbona unaurudisha mkono wako,

Naam, mkono wako wa kulia,

Uutoe kifuani mwako,

Ukawaangamize kabisa.

12 Lakini Mungu ni mfalme wangu tokea zamani,

Afanyaye mambo ya wokovu katikati ya nchi.

13 Wewe umeipasua bahari kwa nguvu zako,

Umevivunja vichwa vya nyangumi juu ya maji.

14 Wewe ulivivunja vichwa vya Lewiathani,

Awe chakula cha watu wa jangwani.

15 Wewe ulitokeza chemchemi na kijito;

Wewe ulikausha mito yenye maji sikuzote.

16 Mchana ni wako, usiku nao ni wako,

Ndiwe uliyeufanya mwanga na jua.

17 Wewe uliiweka mipaka yote ya dunia,

Majira ya joto na ya baridi wewe uliyafanya.

18 Ee BWANA, uyakumbuke hayo, adui amelaumu,

Na watu wapumbavu wamelidharau jina lako.

19 Usimpe mnyama mkali uhai wa njiwa wako;

Usiwasahau milele watu wako walioonewa.

20 Ulitafakari agano lako;

Maana mahali kwenye giza katika nchi

Kumejaa makao ya ukatili.

21 Aliyeonewa asirejee ametiwa haya,

Mnyonge na mhitaji na walisifu jina lako.

22 Ee Mungu, usimame, ujitetee mwenyewe,

Ukumbuke unavyotukanwa na mpumbavu mchana kutwa.

23 Usiisahau sauti ya watesi wako,

Ghasia yao wanaokupinga inapaa daima.

Veja também

Publicidade
Bíblia Online Bíblia Online

Bíblia Online • Versão: 2026-06-16_06-50-08-