Publicidade

Salmos 79

Ombi la Huruma kwa Yerusalemu
Zaburi ya Asafu

1 Ee Mungu, mataifa wameingia katika urithi wako,

Wamelinajisi hekalu lako takatifu.

Wamefanya Yerusalemu chungu chungu.

2 Wameziacha maiti za watumishi wako

Ziwe chakula cha ndege wa angani.

Na miili ya watauwa wako

Iwe chakula cha wanyama wa nchi.

3 Wamemwaga damu yao kama maji

Pande zote za Yerusalemu,

Wala hapakuwa na mtu wa kuwazika.

4 Tumekuwa lawama kwa jirani zetu,

Mzaha na dhihaka kwao wanaotuzunguka.

5 Ee BWANA, hadi lini? Utaona hasira milele?

Wivu wako utawaka kama moto?

6 Ukali wako uwamwagie mataifa wasiokujua,

Na falme za hao wasioliitia jina lako.

7 Kwa maana wamemla Yakobo,

Na makao yake wameyaharibu.

8 Usikumbuke juu yetu maovu ya baba zetu,

Rehema zako zije kutulaki haraka,

Kwa maana tumeteseka sana.

9 Ee Mungu wa wokovu wetu, utusaidie,

Kwa ajili ya utukufu wa jina lako.

Utuokoe, utusamehe dhambi zetu,

Kwa ajili ya jina lako.

10 Kwa nini mataifa yaseme,

Yuko wapi Mungu wao?

Kisasi cha damu ya watumishi wako iliyomwagika

Kijulike kati ya mataifa machoni petu.

11 Kuugua kwake aliyefungwa

Na kuingie mbele zako.

Kwa kadiri ya uweza wa mkono wako

Uwahifadhi waliohukumiwa kufa.

12 Uwalipe jirani zetu mara saba vifuani mwao

Laumu zao walizokulaumu, Ee Bwana.

13 Na sisi tulio watu wako,

Na kondoo za malisho yako,

Tutakushukuru milele;

Tutazisimulia sifa zako kizazi hadi kizazi.

Veja também

Publicidade
Bíblia Online Bíblia Online

Bíblia Online • Versão: 2026-06-15_21-32-39-