1 Tuokoe, ee BWANA, maana hamna tena amchaye Mungu
Maana waaminifu wametoweka katika wanadamu.
2 Husemezana yasiyofaa kila mtu na mwenziwe,
Wenye midomo ya kujipendekeza;
Husemezana kwa mioyo ya unafiki;
3 BWANA ataikata midomo yote ya kujipendekeza,
Na ulimi unenao maneno ya kiburi;
4 Waliosema, Kwa ndimi zetu tutashinda;
Midomo yetu ni yetu wenyewe,
Ni nani aliye bwana juu yetu?
5 Kwa ajili ya kuonewa kwao wanyonge,
Kwa ajili ya kuugua kwao wahitaji,
Sasa nitasimama, asema BWANA,
Nitamweka salama yeye wanayemfyonya.
6 Maneno ya BWANA ni maneno safi,
Ni fedha iliyojaribiwa kalibuni juu ya nchi;
Iliyosafishwa mara saba.
7 Wewe, BWANA, ndiwe utakayetuhifadhi,
Utatulinda na kizazi hiki milele.
8 Wasio haki hutembea pande zote,
Huku ufisadi ukitukuka kati ya wanadamu.