Baraka za Mungu nyumbani
Wimbo wa kupanda mlima.
1 BWANA asipoijenga nyumba
Waijengao wanafanya kazi bure.
BWANA asipoulinda mji
Yeye aulindaye anakesha bure.
2 Kazi yenu ni bure, mnaoamka mapema,
Na kukawia kwenda kulala,
Na kula chakula cha taabu;
Yeye humpa mpenzi wake usingizi.
3 Tazama, watoto ni urithi kutoka kwa BWANA,
Uzao wa tumbo ni thawabu.
4 Kama mishale mkononi mwa shujaa,
Ndivyo walivyo watoto wa ujanani.
5 Heri mtu yule
Aliyelijaza podo lake hivyo.
Naam, hawataona aibu
Wanaposema na adui langoni.