1 Ee Mungu wangu, uniponye na adui zangu,
Uniinue juu yao wanaoshindana nami.
2 Uniponye nao wafanyao maovu,
Uniokoe na watu wa damu.
3 Kwa maana wanaiotea nafsi yangu;
Wenye nguvu wamepanga kunishambulia;
Ee BWANA, si kwa kosa langu,
Wala si kwa hatia yangu.
4 Bila kosa langu wanaenda mbio, kujiweka tayari;
Inuka utazame na kunisaidia.
5 Na Wewe, BWANA, Mungu wa majeshi,
Mungu wa Israeli, uinuke.
Uwapatilize mataifa yote;
Usimrehemu hata mmoja wa wale wapangao maovu kwa hila.
6 Wakati wa jioni hurudi, wakilia kama mbwa,
Na kuzungukazunguka mjini.
7 Tazama, kwa vinywa vyao huteuka,
Midomoni mwao mna panga,
Kwa maana ni nani asikiaye?
8 Na Wewe, BWANA, utawacheka,
Utawadhihaki mataifa yote.
9 Ee nguvu zangu, nitakungoja Wewe,
Maana Mungu ndiye aliye ngome yangu.
10 Mungu wa fadhili zangu atanitangulia,
Mungu atanijalia kutazama kwa ushindi juu ya adui zangu.
11 Usiwaue, watu wangu wasije wakasahau;
Uwatawanye kwa uweza wako,
Na kuwaangamiza, Ee Bwana, ngao yetu.
12 Kwa dhambi ya kinywa chao,
Na kwa neno la midomo yao,
Wanaswe kwa kiburi chao,
Kwa ajili ya kulaani na uongo wasemao.
13 Uwakomeshe kwa hasira,
Uwakomeshe watoweke,
Wajue ya kuwa Mungu atawala katika Yakobo,
Na hata miisho ya dunia.
14 Wakati wa jioni hurudi, wakilia kama mbwa,
Na kuzungukazunguka mjini.
15 Wanatangatanga wakitafuta chakula;
Na kunung'unika wasiposhiba.
16 Nami nitaimba juu ya nguvu zako,
Nitaimba kwa furaha juu ya fadhili zako asubuhi.
Maana umekuwa ngome yangu,
na kimbilio wakati wa mateso yangu.
17 Ee nguvu zangu, nitakuimbia sifa,
Maana Ewe Mungu ndiwe ngome yangu,
Mungu wa fadhili zangu.