1 Ee Mungu, wastahili sifa katika Sayuni,
Na kwako Wewe itaondolewa nadhiri.
2 Wewe usikiaye maombi,
Wote wenye mwili watakujia.
3 Tutakapozidiwa na matendo maovu
Wewe utatuondolea uovu wetu.
4 Heri mtu yule umchaguaye,
Na kumkaribisha akae nyuani mwako.
Na tushibe wema wa nyumba yako,
Patakatifu pa hekalu lako.
5 Kwa mambo ya kutisha utatujibu,
Katika haki, Ee Mungu wa wokovu wetu.
Wewe uliye tumaini la miisho yote ya dunia,
Na la bahari iliyo mbali sana,
6 Milima waiweka imara kwa nguvu zako,
Huku ukijifunga uweza kama mshipi.
7 Watuliza kuvuma kwa bahari,
Kuvuma kwa mawimbi yake,
Na ghasia za watu;
8 Kwa hiyo wakaao mbali kabisa huogopa ishara zako;
Milango ya asubuhi na jioni waifurahisha.
9 Umeijia nchi na kuisitawisha,
Umeitajirisha sana;
Mto wa Mungu umejaa maji;
Wawapa watu nafaka
Maana ndiwe uitengenezaye ardhi.
10 Matuta yake wayajaza maji;
Wapasawazisha palipoinuka,
Wailainisha nchi kwa manyunyu;
Waibariki mimea yake.
11 Umeuvika mwaka taji la wema wako;
Mapito yako yadondoza unono.
12 Huyadondokea malisho ya nyikani,
Na vilima vimejawa na furaha.
13 Na malisho yamejawa na kondoo,
Na mabonde yamepambwa nafaka,
Yanashangilia, na kuimba pamoja kwa shangwe.