Sala ya kupata fadhili za Mungu tena
Kwa mwimbishaji. Ya Wakorahi. Zaburi.
1 Yer 30:18;Eze 39:25 BWANA, umeiridhia nchi yako,
Umewarejesha mateka wa Yakobo.
2 Umeusamehe uovu wa watu wako,
Umezisitiri hatia zao zote.
3 Umeiondoa ghadhabu yako yote,
Umerudi na kuuacha ukali wa hasira yako.
4 Mungu wa wokovu wetu, uturudishe,
Uikomeshe hasira uliyo nayo juu yetu.
5 Je! Utatufanyia hasira hata milele?
Utadumisha ghadhabu kizazi hadi kizazi?
6 Hab 3:2 Je! Hutaki kurudi na kutuhuisha,
Ili watu wako wakufurahie?
7 Ee BWANA, utuoneshe rehema zako,
Utupe wokovu wako.
8 Hab 2:1;Zek 9:10;2 Pet 2:20 Na nisikie atakavyosema Mungu BWANA,
Maana atawaambia watu wake amani,
Naam, na watauwa wake pia,
Bali wasiurudie upumbavu tena.
9 Hakika wokovu wake uko karibu na wamchao,
Ndipo utukufu wake ukae katika nchi yetu.
10 Mik 7:20;Yn 1:17;Zab 72:2,3;Isa 32:17;Lk 2:14;Yn 14:27 Fadhili na kweli zitakutana,
Haki na amani zitakumbatiana.
11 Isa 45:8;2 Kor 5:14-21 Kweli itachipuka katika nchi,
Haki itachungulia kutoka mbinguni.
12 Yak 1:17 Naam, BWANA atatoa kilicho chema,
Na nchi yetu itatoa mazao yake.
13 Haki itakwenda mbele zake,
Na kuzitayarishia hatua zake mapito.