1 BWANA, umkumbukie Daudi
Taabu zake zote alizotaabika.
2 Vile alivyomwapia BWANA,
Akaweka nadhiri kwa ewe Mwenye nguvu wa Yakobo.
3 "Sitaingia nyumbani mwangu,
Wala sitalala kitandani mwangu;
4 Sitaacha macho yangu kuwa na usingizi,
Wala kope zangu kusinzia;
5 Hadi nitakapompatia BWANA mahali,
Na Mwenye nguvu wa Yakobo maskani".
6 Tazama, tulisikia habari zake katika Efrata,
Katika shamba la Yearimu tuliiona.
7 Na tuingie katika maskani yake,
Tusujudu penye kiti cha kuwekea miguu yake.
8 Ee BWANA, uinuke, uende kwenye raha yako,
Wewe na sanduku la nguvu zako.
9 Makuhani wako na wavikwe haki,
Watauwa wako na washangilie.
10 Kwa ajili ya Daudi, mtumishi wako,
Usiurudishe nyuma uso wa masihi wako.
11 BWANA amemwapia Daudi neno la kweli,
Hatarudi nyuma akalivunja,
Mmoja wa wazawa wako mwenyewe
Nitawaweka katika kiti chako cha enzi.
12 Wanao wakiyashika maagano yangu,
Na shuhuda nitakazowafundisha;
Watoto wao nao wataketi
Katika kiti chako cha enzi milele.
13 Kwa kuwa BWANA ameichagua Sayuni,
Ameitamani akae ndani yake.
14 Hapo ndipo mahali pangu pa raha milele,
Hapo nitakaa kwa maana nimepatamani.
15 Hakika nitavibariki vyakula vyake
Wahitaji wake nitawashibisha chakula.
16 Na makuhani wake nitawavika wokovu,
Na watauwa wake watashangilia.
17 Hapo nitamchipushia Daudi pembe,
Na taa nimemtengenezea masihi wangu.
18 Adui zake nitawavika aibu,
Bali juu yake taji lake litasitawi.