Hakikisho la ulinzi wa Mungu
Wimbo wa Upandaji mlima.
1 Nayainua macho yangu niitazame milima,
Msaada wangu utatoka wapi?
2 Msaada wangu hutoka kwa BWANA,
Aliyezifanya mbingu na nchi.
3 Hatauacha mguu wako usogezwe;
Akulindaye hatasinzia;
4 Naam, hatasinzia wala hatalala,
Yeye aliye mlinzi wa Israeli.
5 BWANA ndiye mlinzi wako;
BWANA ni uvuli katika mkono wako wa kulia.
6 Jua halitakupiga mchana,
Wala mwezi wakati wa usiku.
7 BWANA atakulinda na mabaya yote,
Atakulinda nafsi yako.
8 BWANA atakulinda utokapo na uingiapo,
Tangu sasa na hata milele.