1 Ee BWANA, nimekuita, unijie hima,
Uisikie sauti yangu nikuitapo.
2 Sala yangu ipae mbele zako kama uvumba,
Kuinuliwa mikono yangu kama dhabihu ya jioni.
3 Ee BWANA, uweke mlinzi kinywani pangu,
Mngojezi mlangoni pa midomo yangu.
4 Usiuelekeze moyo wangu kunako jambo baya,
Nisiyazoelee matendo yasiyofaa,
Pamoja na watu watendao maovu;
Wala nisile vyakula vyao vya anasa.
5 Mwenye haki na anipige, itakuwa fadhili;
Anikemee, itakuwa kama mafuta kichwani;
Kichwa changu kisikatae,
Maana siachi kusali kati ya mabaya yao.
6 Wakuu wao wakiangushwa kando ya genge,
Watayasikia maneno yangu, maana ni matamu.
7 Kama kupasua kuni na kuzichanja juu ya nchi,
Ndivyo ilivyo mifupa yetu mdomoni pa kuzimu.
8 Macho yangu yanakuelekea Wewe, MUNGU Bwana,
Nimekukimbilia Wewe, usiniache bila kinga.
9 Unilinde kutoka kwa mtego walionitegea,
Na kutoka kwa matanzi ya watendao maovu.
10 Wabaya na waanguke katika nyavu zao wenyewe,
Wakati ninapopita salama.