Publicidade

Salmos 80

Sala ya kurejeshwa kwa Israeli
Kwa mwimbishaji: kwa mtindo wa Yungiyungi, Agano. Ya Asafu. Zaburi.

1 Wewe uchungaye Israeli, usikie,

Wewe umwongozaye Yusufu kama kundi;

Wewe uketiye juu ya makerubi, utoe nuru.

2 Mbele ya Efraimu, na Benyamini, na Manase,

Uziamshe nguvu zako,

Uje, utuokoe.

3 Ee Mungu, uturudishe,

Uangaze uso wako nasi tutaokoka.

4 Ee BWANA, Mungu wa majeshi, hadi lini

Utayaghadhibikia maombi ya watu wako?

5 Umewalisha mkate wa machozi,

Umewanywesha machozi kwa kipimo kikuu.

6 Unatufanya sababu ya ugomvi kwa jirani zetu,

Na adui zetu wanacheka wao kwa wao.

7 Ee Mungu wa majeshi, uturudishe,

Uangaze uso wako nasi tutaokoka.

8 Ulileta mzabibu kutoka Misri,

Ukawafukuza mataifa ukaupanda.

9 Ulitengeneza nafasi mbele yake,

Nao ukatia mizizi sana ukaijaza nchi.

10 Milima ilifunikwa kwa kivuli chake,

Matawi yake ni kama mierezi ya Mungu.

11 Nao uliyaeneza matawi yake hadi baharini,

Na vichipukizi vyake hadi kunako Mto.

12 Kwa nini umezibomoa kuta zake,

Wakauchuma wote wapitao njiani?

13 Nguruwe wa msituni wanauharibu,

Na hayawani wa kondeni wanautafuna.

14 Ee Mungu wa majeshi, tunakusihi, urudi,

Utazame toka juu uone, uujie mzabibu huu.

15 Na mche ule ulioupanda

Kwa mkono wako wa kulia;

Na tawi lile ulilolifanya

Kuwa imara kwa nafsi yako.

16 Umechomwa moto; umekatwa;

Kwa lawama ya uso wako wanapotea.

17 Mkono wako na uwe juu yake

Mtu aliye katika mkono wako wa kulia;

Juu ya mwanadamu uliyeimarisha

Kwa nafsi yako;

18 Kisha hatutakuacha kwa kurudi nyuma;

Utuhuishe nasi tutaliitia jina lako.

19 Ee BWANA, Mungu wa majeshi, uturudishe,

Uangaze uso wako nasi tutaokoka.

Veja também

Publicidade
Bíblia Online Bíblia Online

Bíblia Online • Versão: 2026-06-16_18-40-07-