Sifa kwa wema wa Mungu kwa Israeli
1 Haleluya.
Mwimbieni BWANA wimbo mpya,
Sifa zake katika kusanyiko la watauwa.
2 Israeli na amfurahie Yeye aliyemwumba,
Wana wa Sayuni na wamshangilie mfalme wao.
3 Na walisifu jina lake kwa kucheza,
Kwa sauti tamu ya matari na kinubi.
4 Kwa kuwa BWANA awaridhia watu wake,
Huwapamba wenye upole kwa wokovu.
5 Watauwa na waushangilie utukufu,
Waimbe kwa sauti kuu vitandani mwao.
6 Sifa kuu za Mungu na ziwe vinywani mwao,
Na upanga mkali kuwili mikononi mwao.
7 Ili kufanya kisasi juu ya mataifa,
Na adhabu juu ya makabila ya watu.
8 Wawafunge wafalme wao kwa minyororo,
Na wakuu wao kwa pingu za chuma.
9 Kuwafanyia hukumu iliyoandikwa;
Hiyo ndiyo heshima ya watauwa wake wote.
Haleluya.