Publicidade

Salmos 31

Sala na sifa kwa kukombolewa kutoka kwa adui
Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi.

1 Nimekukimbilia Wewe, BWANA,

Nisiaibike milele.

Kwa haki yako uniponye,

2 Unitegee sikio lako, uniokoe hima.

Uwe kwangu mwamba wa nguvu,

Ngome thabiti ya kuniokoa.

3 Ndiwe mwamba wangu na ngome yangu;

Kwa ajili ya jina lako uniongoze na unichunge.

4 Utanitoa katika wavu walionitegea kwa siri,

Maana Wewe ndiwe ngome yangu.

5 Mikononi mwako naiweka roho yangu;

Umenikomboa, Ee BWANA, Mungu wa kweli.

6 Nawachukia wao washikao yasiyofaa yenye uongo;

Bali mimi namtumainia BWANA.

7 Na nishangilie, nizifurahie fadhili zako,

Kwa kuwa umeyaona mateso yangu.

Umeijua nafsi yangu taabuni,

8 Wala hukunitia mikononi mwa adui;

Miguu yangu umeisimamisha mahali penye usalama.

9 Ee BWANA, unifadhili, maana ni katika dhiki,

Jicho langu limenyauka kwa masumbufu,

Naam, mwili wangu na nafsi yangu.

10 Maana maisha yangu yamekwisha kwa huzuni,

Na miaka yangu kwa maumivu.

Nguvu zangu zimeniishia kwa uovu wangu,

Na mifupa yangu imepooza.

11 Kwa sababu ya watesi wangu nimelaumiwa,

Naam, hasa kwa jirani zangu;

Na kitu cha kutisha kwa rafiki zangu;

Wanaoniona njiani wananikimbia.

12 Nimesahauliwa kama mfu asiyekumbukwa;

Nimekuwa kama chombo kilichovunjika.

13 Maana nimesikia wengi wakinong'onezana;

Hofu katika pande zote.

Waliposhauriana juu yangu,

Walipanga kunitoa uhai wangu.

14 Lakini mimi nakutumaini Wewe, BWANA,

Nimesema, Wewe ndiwe Mungu wangu.

15 Nyakati zangu zimo mikononi mwako;

Uniponye kutoka kwa adui zangu na wanaonifuatia.

16 Umwangaze mtumishi wako

Kwa nuru ya uso wako;

Uniokoe kwa ajili ya fadhili zako.

17 Ee BWANA, nisiaibishwe, maana nimekuita;

Waaibishwe wasio haki, wanyamaze kuzimuni.

18 Midomo ya uongo iwe na ububu,

Imneneayo mwenye haki maneno ya kiburi,

Kwa majivuno na dharau.

19 Jinsi zilivyo nyingi fadhili zako

Ulizowawekea wakuchao;

Ulizowatendea wakukimbiliao

Mbele ya wanadamu!

20 Utawasitiri kutoka kwa fitina za watu

Katika maficho ya kuwapo kwako;

Utawaficha katika hema

Na ushindani wa ndimi.

21 BWANA ahimidiwe; kwa maana amenitendea

Fadhili za ajabu nilipozongwa kama mji wenye boma.

22 Nami nilisema kwa pupa yangu,

Nimekatiliwa mbali na macho yako;

Lakini ulisikia sauti ya kilio changu

Wakati nilipokulilia.

23 Mpendeni BWANA,

Ninyi nyote mlio watauwa wake.

BWANA huwahifadhi waaminifu,

Bali humlipiza mwenye kiburi ipasavyo.

24 Iweni hodari, na mpige moyo konde,

Ninyi nyote mnaomngoja BWANA.

Veja também

Publicidade
Bíblia Online Bíblia Online

Bíblia Online • Versão: 2026-06-16_06-50-08-