Ukuu wa enzi ya Mungu
1 BWANA ametamalaki, amejivika adhama,
BWANA amejivika, ukuu na nguvu, kama mavazi ya kifalme.
Naam, ulimwengu umethibitika usitikisike;
2 Kiti chako kimekuwa thabiti tokea zamani;
Wewe ndiwe uliye tangu milele.
3 Ee BWANA, mito imepaza,
Mito imepaza sauti zake,
Mito imepaza uvumi wake.
4 Kupita sauti ya maji mengi, maji makuu,
Kupita mawimbi ya bahari yaumkayo,
BWANA Aliye Juu ndiye mwenye ukuu.
5 Shuhuda zako ni amini sana;
Utakatifu ndio uifaao nyumba yako,
Ee BWANA, milele na milele.