Wimbo wa sifa na sala kwa Yerusalemu
Wimbo wa kupanda mlima.
1 Nilifurahi waliponiambia,
Twende nyumbani kwa BWANA.
2 Miguu yetu imesimama
Ndani ya malango yako, Ee Yerusalemu.
3 Ee Yerusalemu uliyejengwa
Kama mji ulioshikamana,
4 Huko ndiko wapandako kabila,
makabila ya BWANA;
Kama ulivyowaamuru Waisraeli,
Walishukuru jina la BWANA.
5 Maana huko viliwekwa viti vya hukumu,
Viti vya enzi vya ukoo wa Daudi.
6 Uombeeni Yerusalemu amani;
Na wafanikiwe wakupendao;
7 Amani na ikae ndani ya kuta zako,
Na kufanikiwa ndani ya majumba yako.
8 Kwa ajili ya ndugu zangu na rafiki zangu
Niseme sasa, Amani ikae nawe.
9 Kwa ajili ya nyumba ya BWANA, Mungu wetu,
Nitakuombea mema.