1 Nimpazie Mungu sauti yangu,
Naam, nimpazie Mungu, naye atanisikia.
2 Katika siku ya taabu yangu nilimtafuta Bwana;
Mkono wangu ulinyoshwa usiku, bila kulegea;
Nafsi yangu ilikataa kufarijika.
3 Nilipotaka kumkumbuka Mungu nilifadhaika;
Nilipotaka kutafakari roho yangu ilizimia.
4 Ulizishika kope za macho yangu zisifumbike;
Nilitaabika nisiweze kunena.
5 Nilifikiri habari za siku za kale,
Miaka ya zamani zilizopita.
6 Nanena na moyo wangu usiku,
Nawaza moyoni mwangu,
Roho yangu naipeleleza.
7 Je! Bwana atatutupa milele na milele?
Asiwe na fadhili kwetu kamwe?
8 Rehema zake zimekoma hata milele?
Ahadi yake imekwisha hata vizazi vyote?
9 Mungu amesahau fadhili zake?
Amezuia kwa hasira rehema zake?
10 Nikasema, Ndio udhaifu wangu huo;
Lakini nitaikumbuka miaka ya mkono wa kulia wake Aliye Juu.
11 Nitayakumbuka matendo ya BWANA;
Naam, nitayakumbuka maajabu yako ya kale.
12 Pia nitaitafakari kazi yako yote;
Nitaziwaza habari za matendo yako.
13 Ee Mungu, njia yako iko katika utakatifu;
Ni Mungu yupi aliye mkuu kama Mungu wetu?
14 Wewe ndiwe Mungu ufanyaye maajabu;
Uliudhihirisha uweza wako kati ya mataifa.
15 Kwa mkono wako umewakomboa watu wako,
Wana wa Yakobo na Yusufu.
16 Ee Mungu, yale maji yalikuona,
Yale maji yalikuona, yakaogopa.
Vilindi vya maji navyo vikatetemeka,
17 Mawingu yakamwaga maji.
Mbingu nazo zikatoa sauti,
Mishale yako nayo ikatapakaa.
18 Sauti ya radi yako ikawa katika kisulisuli;
Umeme uliuangaza ulimwengu.
Nchi ilitetemeka na kutikisika;
19 Njia yako ilikuwa katika bahari.
Na mapito yako yalikuwa katika maji makuu;
Hatua zako hazikujulikana.
20 Uliwaongoza watu wako kama kundi,
Kwa mkono wa Musa na Haruni.