Publicidade

Salmos 7

Ombi la msaada juu ya watesaji
Ombolezo la Daudi, aliloimba kwa BWANA kuhusu Kushi, Mbenyamini.

1 BWANA, Mungu wangu, nimekukimbilia Wewe,

Uniokoe na wote wanaonifuatia, uniponye.

2 Asije akaipapura nafsi yangu kama simba,

Akaniburura hadi pasipokuwa na wa kuniponya.

3 BWANA, Mungu wangu, ikiwa nimetenda haya,

Ikiwa mna uovu mikononi mwangu,

4 Ikiwa nimemlipa mabaya

Yeye aliyekaa kwangu salama;

(Hasha! Nimemponya yeye

Aliyekuwa mtesi wangu bila sababu;)

5 Basi adui na anifuatie,

Na kuikamata nafsi yangu;

Naam, aukanyage uzima wangu,

Na kuulaza utukufu wangu mavumbini.

6 BWANA uondoke kwa hasira yako;

Ujiinue Juu ya ujeuri wa watesi wangu;

Uamke kwa ajili yangu;

Umeamuru hukumu.

7 Kusanyiko la mataifa na likuzunguke,

Na juu yake uketi utawale.

8 BWANA atawaamua mataifa,

BWANA, unihukumu mimi,

Kwa kadiri ya haki yangu,

Kulingana na unyofu nilio nao.

9 Ubaya wao wasio haki na ukome,

Lakini umthibitishe mwenye haki.

Kwa maana mjaribu mioyo na fikira

Ndiye Mungu aliye mwenye haki.

10 Ngao yangu ina Mungu,

Awaokoaye wanyofu wa moyo.

11 Mungu ni mwamuzi mwenye haki,

Naam, Mungu akasirikiaye waovu kila siku.

12 Mtu asipoongoka ataunoa upanga wake;

Ameupinda uta wake na kuuweka tayari;

13 Naye amemtengenezea silaha za kuua,

Akifanya mishale yake kuwa mipini ya moto.

14 Tazama, huyu ametunga uovu,

Amechukua mimba ya madhara, amezaa uongo.

15 Amechimba shimo, amelichimba chini sana,

Akatumbukia katika handaki aliyoichimba!

16 Madhara yake yatamrejea kichwani pake,

Na dhuluma yake itamshukia utosini.

17 Nitamshukuru BWANA kwa kadiri ya haki yake;

Nitaliimbia jina la BWANA aliye juu.

Veja também

Publicidade
Bíblia Online Bíblia Online

Bíblia Online • Versão: 2026-06-16_18-40-07-