Nani atakaa katika patakatifu pa Mungu?
Zaburi ya Daudi.
1 BWANA, ni nani atakayekaa
Katika hema yako?
Ni nani atakayeishi
Katika kilima chako kitakatifu?
2 Ni mtu aendaye kwa ukamilifu,
Na kutenda haki.
Asemaye kweli kwa moyo wake,
3 Asiyesingizia kwa ulimi wake.
Wala kumtenda mwenziwe mabaya,
Wala kumsengenya jirani yake.
4 Anayedharau waovu Machoni pake,
Bali huwaheshimu wamchao BWANA
Aliyeapa ingawa kwa hasara yake,
Hayabadili maneno yake.
5 Asiyetoa fedha yake apate kula riba,
Asiyepokea rushwa amwangamize asiye na hatia.
Mtu atendaye mambo hayo
Hataondoshwa milele.