1 Ee BWANA, utege sikio lako unijibu,
Maana mimi ni maskini na mhitaji.
2 Unihifadhi nafsi yangu,
Maana mimi ni mcha Mungu.
Wewe uliye Mungu wangu,
Umwokoe mtumishi wako anayekutumaini.
3 Wewe, Bwana, unifadhili,
Maana nakulilia Wewe mchana kutwa.
4 Uifurahishe nafsi ya mtumishi wako,
Maana nafsi yangu nakuinulia Wewe, Bwana.
5 Kwa maana Wewe, Bwana, U mwema,
Umekuwa tayari kusamehe,
Na mwingi wa fadhili,
Kwa watu wote wakuitao.
6 Ee BWANA, uyasikie maombi yangu;
Uisikilize sauti ya dua zangu.
7 Siku ya mateso yangu nitakuita,
Kwa maana utaniitikia.
8 Katikati ya miungu hakuna kama Wewe, Bwana,
Wala matendo mfano wa matendo yako.
9 Mataifa yote uliyoyaumba watakuja;
Watakusujudia Wewe, Bwana,
Watalitukuza jina lako;
10 Kwa kuwa ndiwe uliye mkuu,
Wewe ndiwe mfanya miujiza,
Ndiwe Mungu peke yako.
11 Ee BWANA, unifundishe njia yako;
Nitakwenda katika kweli yako;
Moyo wangu na ufurahi kulicha jina lako;
12 Nitakusifu Wewe, Ee Bwana, Mungu wangu,
Kwa moyo wangu wote,
Nitalitukuza jina lako milele.
13 Maana fadhili zako kwangu ni nyingi sana;
Umeiopoa nafsi yangu na kuzimu.
14 Ee Mungu, wenye kiburi wamenishambulia;
Kundi la watu wakatili wanataka kuniua.
Wala hawakukuweka Wewe
Mbele ya macho yao.
15 Lakini Wewe, Bwana,
U Mungu wa rehema na neema,
Mvumilivu, mwingi wa fadhili na kweli.
16 Unielekee na kunifadhili mimi;
Mpe mtumishi wako nguvu zako,
Umwokoe mwana wa mjakazi wako.
17 Unifanyie ishara ya wema,
Wanichukiao waione na kuaibishwa.
Kwa kuwa Wewe, BWANA,
Umenisaidia na kunifariji.