Ombi la Mungu kwa Waisraeli wakaidi
Kwa mwimbishaji: kwa mtindo wa Gitithi. Ya Asafu.
1 Mwimbieni Mungu, nguvu zetu, nyimbo za furaha,
Mshangilieni Mungu wa Yakobo.
2 Pazeni zaburi, pigeni matari,
Kinubi chenye sauti nzuri, na kinanda.
3 Hes 10:10 Pigeni panda mwandamo wa mwezi,
Kukiwa na mbalamwezi, wakati wa sikukuu yetu.
4 Law 23:24;Hes 10:10 Kwa maana ni sheria kwa Israeli,
Ni hukumu ya Mungu wa Yakobo.
5 Aliamuru iwe ushuhuda katika Yusufu,
Alipoondoka juu ya nchi ya Misri;
Maneno yake nisiyemjua niliyasikia.
6 Nimeutua mzigo begani mwake;
Mikono yake nikaiondolea kazi nzito.
7 Kut 17:7;Hes 20:13 Katika shida uliniita nikakuokoa;
Nilikuitikia kutoka maficho yangu ya radi;
Nilikujaribu penye maji ya Meriba.
8 Enyi watu wangu, sikieni, nami nitawaonya,
Ee Israeli, kama ukitaka kunisikiliza;
9 Kut 20:2-3;Kum 5:6-7 Usiwe na mungu mgeni ndani yako;
Wala usimsujudie mungu mwingine.
10 Zab 37:3;Yn 15:7 Mimi ndimi BWANA, Mungu wako,
Niliyekupandisha toka nchi ya Misri;
Fumbua sana kinywa chako nami nitakijaza.
11 Lakini watu wangu hawakuisikiliza sauti yangu,
Wala Israeli hawakunitaka.
12 Mdo 7:42;Rum 1:24 Nikawaacha wakaenda kwa ukaidi wa mioyo yao,
Waenende katika mashauri yao.
13 Kum 5:29;Isa 48:18;Yer 44:4,5;Mt 23:37 Laiti watu wangu wangenisikiliza,
Na Israeli angeenenda katika njia zangu;
14 Ningewadhili adui zao kwa upesi,
Na juu ya watesi wao ningegeuza mkono wangu;
15 Wamchukiao BWANA wangenyenyekea mbele zake,
Na maangamizi yao yangedumu milele.
16 Naam, ningewalisha kwa ngano iliyo bora zaidi,
Ningewashibisha kwa asali itokayo mwambani.