Zaburi. Wimbo wa siku ya Sabato.
1 Ni neno jema kumshukuru BWANA,
Na kuliimbia jina lako sifa, Ee Uliye Juu.
2 Kuzitangaza rehema zako asubuhi,
Na uaminifu wako wakati wa usiku.
3 Kwa chombo chenye nyuzi kumi,
Na kwa kinanda,
Na kwa mlio wa kinubi.
4 Kwa kuwa umenifurahisha, BWANA,
Kwa kazi yako; nitashangilia
Kwa ajili ya matendo ya mikono yako.
5 Isa 28:29;Rum 11:23 Ee BWANA, jinsi yalivyo makuu matendo yako!
Mawazo yako ni mafumbo makubwa.
6 Zab 73:22 Mtu mjinga hayatambui hayo,
Wala mpumbavu hayafahamu.
7 Ayu 21:7;Yer 12:1;Mal 3:15 Hata wasio haki wakichipuka kama majani
Na wote watendao maovu wakastawi.
Mwishowe wataangamizwa milele;
8 Bali Wewe, BWANA, U Mtukufu hata milele.
9 Maana hao adui zako, Ee BWANA,
Hao adui zako watapotea,
Na watendao maovu watatawanyika wote pia.
10 Bali pembe yangu umeiinua kama pembe ya nyati,
Nimepakwa mafuta mabichi.
11 Na jicho langu limeona kuanguka kwa adui zangu,
Sikio langu limesikia maangamizi ya waovu walionishambulia.
12 Zab 52:8;Wim 7:7 Mwenye haki atastawi kama mtende,
Atakua kama mwerezi wa Lebanoni.
13 Isa 60:21;Mt 15:13;Yn 15:2,5 Waliopandwa katika nyumba ya BWANA
Watastawi katika nyua za Mungu wetu.
14 Watazaa matunda hadi wakati wa uzee,
Watajaa utomvu, watakuwa na ubichi.
15 Kum 32:4;Rum 9:14 Watangaze ya kuwa BWANA ni mwenye adili,
Mwamba wangu, ndani yake hamna udhalimu.