Sala ya ukombozi kutoka kwa watesi
Utenzi wa Daudi. Alipokuwa pangoni. Ombi.
1 1 Sam 22:1;24:3 Kwa sauti yangu nitamlilia BWANA,
Kwa sauti yangu nitamwomba BWANA dua.
2 Nitafunua mbele zake malalamiko yangu,
Shida yangu nitaitangaza mbele zake.
3 Roho yangu inapozimia unayajua mapito yangu;
Katika njia niendayo wamenifichia mtego.
4 Utazame mkono wangu wa kulia ukaone,
Kwa maana sina mtu anijuaye.
Makimbilio yamenipotea,
Hakuna wa kunitunza roho.
5 Omb 3:24 BWANA, nimekuita nikasema, Ndiwe kimbilio langu,
Fungu langu katika nchi ya walio hai.
6 Zab 116:6;7:1 Ukisikilize kilio changu,
Kwa maana nimedhilika sana.
Uniponye kutoka kwa wanaonifuatia,
Kwa maana wao ni hodari kuliko mimi.
7 Zab 34:2;119:17 Uitoe nafsi yangu kifungoni.
Nipate kulishukuru jina lako.
Wenye haki watanizunguka,
Kwa kuwa Wewe unanikirimu.