Ya Daudi.
1 BWANA ni nuru yangu na wokovu wangu,
Nimwogope nani?
BWANA ni ngome ya uzima wangu,
Nimhofu nani?
2 Watenda mabaya waliponikaribia,
Wanile nyama yangu,
Watesi wangu na adui zangu,
Walijikwaa wakaanguka.
3 Jeshi lijapojipanga kupigana nami,
Moyo wangu hautaogopa.
Vita vijaponitokea,
Hata hapo nitatumainia BWANA.
4 Neno moja nimelitaka kwa BWANA,
Nalo ndilo nitakalolitafuta,
Nikae nyumbani mwa BWANA
Siku zote za maisha yangu,
Niutazame uzuri wa BWANA,
Na kutafakari hekaluni mwake.
5 Mit 18:10;Isa 4:6;Kol 3:3 Maana atanisitiri bandani mwake siku ya mabaya,
Atanisitiri katika sitara ya hema yake,
Na kuniinua juu ya mwamba.
6 Na sasa kichwa changu kitainuka
Juu ya adui zangu wanaonizunguka.
Nami nitatoa dhabihu za shangwe hemani mwake;
Nitaimba, naam, nitamhimidi BWANA.
7 Ee BWANA, usikie, kwa sauti yangu ninalia,
Unifadhili, unijibu.
8 Uliposema, "Nitafuteni uso wangu,"
Moyo wangu umekuambia,
BWANA, uso wako nitautafuta.
9 Usinifiche uso wako,
Usimkatalie mtumishi wako kwa hasira.
Umekuwa msaada wangu, usinitupe,
Wala usiniache, Ee Mungu wa wokovu wangu.
10 Isa 49:15;Yn 16:32;2 Tim 4:16-18 Hata baba yangu na mama yangu wakiniacha,
Bali BWANA atanikaribisha kwake.
11 Ee BWANA, unifundishe njia yako,
Na kuniongoza katika njia iliyonyoka;
Kwa sababu yao wanaoniotea;
12 1 Sam 22:9;Mt 26:59,60 Usinitie katika nia ya watesi wangu;
Maana mashahidi wa uongo wamenijia,
Nao watoao jeuri kama pumzi.
13 Zab 112:7,8 Naamini ya kuwa nitauona wema wa BWANA
Katika nchi ya walio hai.
14 Zab 62:1,5;Isa 25:9;Hab 2:3 Umtumainie BWANA, uwe imara,
Upige moyo konde, naam, umngoje BWANA.